Jopo la wizara ya afya ya Japani limeidhinisha dawa ya kutibu mafua kutumika kutibu ugonjwa unaoenezwa na kupe

Jopo la wataalamu wa wizara ya afya ya Japani limeidhinisha matumizi zaidi ya dawa ya kutibu mafua, Avigan, kutibu ugonjwa wa virusi vinayoenezwa na kupe unaojulikana kama homa kali inayoambatana na upungufu wa chembe sahani za damu, SFTS.

Mara tu wizara itakapozindua rasmi dawa hiyo, itakuwa dawa ya kwanza duniani ya kutibu SFTS.

Wagonjwa walio na SFTS mara nyingi hupata maambukizi ya virusi hao kwa kuumwa na kupe. Dalili ni pamoja na homa na kuhara, lakini hakuna dawa bora inayopatikana kwa sasa.

Wizara ya afya inasema hadi asilimia 30 ya visa vya SFTS nchini Japani vimesababisha vifo.

Avigan ilitengenezwa na kampuni ya Fujifilm Toyama Chemical. Kampuni hiyo iliomba idhini ya wizara ya afya kwa matumizi ya dawa hiyo dhidi ya SFTS mwezi Agosti mwaka jana, ikisema kuwa imepata takwimu za kitafiti juu ya ufanisi wake.

Jana Ijumaa, jopo la wizara ya afya lilithibitisha kuwa dawa hiyo ni nzuri na kwamba hakuna wasiwasi mkubwa juu ya usalama wake.

Awali Avigan iliidhinishwa kama dawa ya kutibu mafua nchini Japani mwaka 2014, na inahifadhiwa na serikali.

Dawa hiyo haiwezi kutumiwa na mama wajawazito au wanawake ambao wanatarajia kuwa wajawazito, kwakuwa utafiti kwa wanyama ulionyesha kuwa inaweza kusababisha ulemavu kwa mtoto ambaye hajazaliwa.