Israel yaapa kuendelea na operesheni mjini Rafah kabla ya uamuzi wa ICJ leo Ijumaa

Israel imeapa kuendelea na operesheni zake mjini Rafah kusini mwa Ukanda wa Gaza huku Mahakama ya Kimataifa ya Haki, ICJ ikitarajiwa kutoa uamuzi leo Ijumaa kuhusu ombi la kuchukuliwa kwa hatua za dharura kusitisha operesheni hizo.

ICJ ilitangaza jana Alhamisi kuwa itatoa agizo lake juu ya ombi la Afrika Kusini la kuitaka Israel kusitisha operesheni zake mjini Rafah. Watu wengi waliohama makwao wametafuta hifadhi mjini humo.

Msemaji wa serikali ya Israel alisema jana Alhamisi kuwa, “Hakuna nguvu yoyote ya Duniani itakayoizuia Israel kuwalinda watu wake na kuwasaka wapiganaji wa kundi la Hamas katika eneo la Gaza.”

Mamlaka za afya za eneo hilo zinasema idadi ya vifo kutokana na mapigano katika eneo la Gaza imepanda hadi 35,800.

Afrika Kusini iliwasilisha kesi katika mahakama ya ICJ baada ya kuituhumu Israel kwa kutekeleza mauaji ya kimbari katika eneo la Gaza.

Mwezi Januari mwaka huu, mahakama hiyo iliiagiza Israel kuchukua hatua zote kuzuia vitendo vya mauaji ya kimbari.

Israel imeitikia vikali maamuzi ya awali ya ICJ.