Putin aweka hatua za kukabiliana na uwezekano wa mali za Urusi kushikiliwa na Marekani

Rais wa Urusi Vladimir Putin amesaini amri inayoruhusu kushikiliwa kwa mali za Marekani zilizopo nchini Urusi iwapo Marekani itataifisha mali za Urusi zilizoshikiliwa chini ya vikwazo.

Amri hiyo inaelezea kwamba mali za Marekani ikiwa ni pamoja na majengo na amana za raia wake nchini Urusi zinaweza kutumiwa kulipa fidia kwa uharibifu unaotokana na kushikiliwa kwa mali za Urusi nchini Marekani. Jopo la serikali litaamua ni mali zipi zitakazojumuishwa kufuatia agizo la mahakama.

Marekani imepitisha sheria zinazoiruhusu kushikilia mali za Urusi zilizopo nchini Marekani kama hatua ya kuiunga mkono Ukraine.

Jumanne wiki hii, nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya zilikubaliana kutumia faida zinazotokana na mali za Benki Kuu ya Urusi kwa ajili ya msaada wa kijeshi kwa Ukraine na malengo mengine.

Mawaziri wa Fedha na Magavana wa Benki Kuu wa Kundi la Nchi Saba zilizoendelea zaidi kiviwanda duniani, G7 wanatarajiwa kujadili suala hilo kwenye mikutano iliyopangwa kuanza leo Ijumaa nchini Italia.