Taiwan yachukua tahadhari kufuatia mazoezi ya kijeshi ya China

Jeshi la Taiwan na kikosi cha walinzi wa pwani wapo katika hali ya tahadhari kufuatia mazoezi ya kijeshi yanayoendelea ya China jirani na Taiwan.

Kamandi ya Eneo la Mashariki ya China ilisema jana Alhamisi kuwa itafanya mazoezi ya kijeshi karibu na Taiwan, Visiwa vya Kinmen na maeneo mengine kwa siku mbili hadi leo Ijumaa.

Msemaji wa Ofisi ya Masuala ya Taiwan ya Baraza la Taifa la China, Chen Binhua alitoa taarifa jana Alhamisi usiku.

Chen alisema hatua za kulipiza kisasi za China zinalenga shughuli zinazopendelea uhuru katika eneo la Taiwan na uingiliaji wa kigeni, lakini kamwe si kwa wazalendo wengi wa Taiwan.

Utawala wa Rais mpya wa Taiwan Lai Ching-te aliyeingia mamlakani Jumatatu wiki hii, ulikataa kutambua kanuni ya “China-moja.”

Wizara ya Ulinzi ya Taiwan ilisema ndege za kijeshi 49 za China zilipita jirani na Taiwan kati ya asubuhi na saa mbili usiku jana Alhamisi.

Wizara hiyo pia ilisema ndege za jeshi na meli za China zilikaribia eneo linalopakana na Taiwan. Kingo za maeneo kama hayo ni takribani kilomita 44 kutoka ukanda wa pwani.

Lakini wizara hiyo iliongeza kuwa jeshi la Taiwan na kikosi cha walinzi wa pwani vilizuia ndege na meli za China kusonga mbele zaidi.