Jeshi la Marekani kwa mara ya kwanza kufanya sehemu ya mazoezi makubwa nchini Japani

NHK imebaini kuwa jeshi la Marekani kwa mara ya kwanza litafanya sehemu yake ya mazoezi makubwa nchini Japani katika jitihada za wazi za kuboresha uwezo wake wa kuitikia haraka ili kushughulikia dharura zinazoweza kutokea karibu na nchi hiyo.

Jeshi la Marekani hufanya mazoezi hayo yanayojulikana kama Valiant Shield mara moja kila baada ya miaka miwili huko Guam na kwingineko.

Mazoezi hayo ya mwaka huu yamepangwa kuanza mapema mwezi Juni na kuendelea kwa karibu wiki mbili.

Vyanzo vya habari vinasema ndege za kijeshi za Marekani zimepangiwa kuwasili kwenye kambi za Marekani na kambi mbili za Kikosi cha Kujihami, SDF nchini Japani ili kufanya mazoezi hayo pamoja na ndege za SDF.

Vyanzo hivyo vinasema kambi hizo mbili za SDF huenda ni Kambi ya Anga ya Hachinohe mkoani Aomori na Kambi ya Anga ya Matsushima mkoani Miyagi.

Kambi hizo za SDF zilizopo kaskazini mashariki mwa Japani zina ndege za kushika doria, ndege za vita na ndege zingine.