Korea Kusini, China na Japani kufanya mkutano wa viongozi wakuu mjini Seoul Jumatatu

Viongozi wakuu wa Korea Kusini, China na Japani watafanya mkutano wa pande tatu mjini Seoul Jumatatu ijayo. Mkutano huo utakuwa wa kwanza katika kipindi cha miaka minne na nusu.

Ofisi ya Rais wa Korea Kusini jana Alhamisi ilisema kuwa Rais Yoon Suk-yeol pia atafanya mazungumzo ya pande mbili na Mawaziri Wakuu Li Qiang wa China na Kishida Fumio wa Japani keshokutwa Jumapili.

Ofisi hiyo iliongeza kuwa mada za mazungumzo hayo zitajumuisha uchumi, mabadilishano ya watu, teknolojia ya kidijitali na ushirikiano wakati wa majanga. Ilisema tamko la pamoja huenda likatolewa mwishoni mwa mkutano wa viongozi hao.

Nchi hizo tatu za bara la Asia zilikuwa zimekubaliana kufanya mkutano wa viongozi wakuu kila mwaka kuanzia mwaka 2008 ili kuimarisha ushirikiano wa kikanda. Lakini mpango huo ulivurugwa na mivutano kati ya Japani na Korea Kusini na janga la virusi vya korona. Mkutano wa mwisho wa viongozi wakuu wa nchi hizo tatu ulifanyika mwezi Disemba mwaka 2019.