Jeshi la China lafanya mazoezi karibu na Taiwan

Jeshi la China limetangaza kwamba limefanya mazoezi ya kijeshi karibu na Taiwan leo Alhamisi asubuhi.

Kamandi ya Eneo la Mashariki ya China ilisema mazoezi hayo yalianza saa 1:45 asubuhi kwa saa za eneo hilo karibu na Kisiwa cha Kinmen na katika maeneo mengine. Pia imesema mazoezi hayo ya kijeshi yanafanyika leo Alhamisi na kesho Ijumaa. Jeshi la China la vikosi vya ardini, majini, anga na vikosi vya roketi vinashiriki.

Kamandi hiyo ilisema wanaotaka uhuru wa Taiwan ni genge la waasi. Ilisema mazoezi hayo ni onyo kali dhidi ya uingiliaji wa vikosi vya nje na magenge ya waasi.

China inazidisha shinikizo kwa utawala wa Taiwan. Rais Lai, ambaye ameingia madarakani Jumatatu wiki hii, amesema hatatambua kanuni ya China moja.