Waziri Mkuu wa Uingereza Sunak aitisha uchaguzi mkuu tarehe 4 Julai

Waziri Mkuu wa Uingereza Rishi Sunak ametangaza uchaguzi mkuu utafanyika Julai 4 huku chama chake cha Conservative kikikabiliwa na changamoto kubwa kwa utawala wake wa miaka 14.

Sunak alitoa tangazo hilo nje ya ofisi ya waziri mkuu Downing Street jana Jumatano. Alisema, "Sasa ni wakati wa Uingereza kuchagua mustakabali wake."

Uchaguzi mkuu ujao ulitakiwa kufanyika kufikia Januari mwakani na ilisubiriwa sana ni lini Sunak angeamua kuomba kuvunjwa kwa bunge na kuitisha uchaguzi.

Chama cha Conservative kimekuwa madarakani tangu mwaka 2010. Lakini kutoridhika kwa umma na serikali kumekuwa kukiongezeka hivi karibuni.

Uingereza iliondoka kwenye Umoja wa Ulaya mwaka 2020, na watu wengi nchini humo wanahisi maisha yao bado hayajaboreka.

Sunak alichukua wadhifa huo mnamo 2022. Kura za maoni mwezi huu zinaonyesha Chama cha Conservative kipo nyuma ya Chama kikuu cha upinzani cha Labour kwa zaidi ya alama 20 katika viwango vya uungaji mkono.