Mazishi ya Raisi na wengine waliouawa katika ajali ya helikopta yafanyika Tehran

Mazishi makubwa yamefanyika katika mji mkuu wa Iran, Tehran, jana Jumatano ya hayati Rais Ebrahim Raisi na wengine waliouawa katika ajali ya helikopta iliyotokea Jumapili iliyopita.

Helikopta hiyo ilianguka kwenye jimbo la kaskazini magharibi mwa Iran Azerbaijan Mashariki. Watu wote wanane waliokuwa kwenye helikopta hiyo, akiwemo Raisi na Waziri wa mambo ya Nje Hossein Amir Abdollahian, walipoteza maisha.

Wawakilishi kutoka mataifa mengi, hususani ya jirani walihudhuria mazishi hayo.

Makamu wa Kwanza wa Rais Mohammad Mokhber, ambaye amechukua wadhifa kama kaimu rais, aliwasalimia wahudhuriaji.

Kutoka China, Naibu Waziri Mkuu Zhang Guoqing alihudhuria. Kutoka Urusi, Mwenyekiti wa baraza la chini la bunge Vyacheslav Volodin alishiriki.

Iran inaonekana ilitaka kuonyesha kwamba uhusiano wake wa kidiplomasia na nchi zingine upo thabiti licha ya vifo visivyotarajiwa vya rais wa nchi na waziri wa mambo ya nje.

Washiriki pia walijumuisha Ismail Haniyeh, kiongozi mwandamizi wa kundi la Kiislamu la Hamas, wanachama waandamizi wa kundi la Waiislamu wa Shia la Lebanon, Hezbollah na waasi wa Houthi wa Yemen miongoni mwa wengine. Makundi hayo yanaungwa mkono na Iran.