Afisa mkuu UNHCR ahimiza uungwaji mkono zaidi kwa watu waliokimbia makazi yao

Afisa mwandamizi wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR ametoa wito wa uelewa mkubwa wa suala la wakimbizi na kuendelea kuwasaidia watu waliokimbia makazi yao.

Naibu Kamishna Mkuu wa UNHCR Kelly Clements alizungumza na NHK jijini Tokyo jana Jumatano.

Mwaka jana UN ilikadiria kuwa takriban watu milioni 114 walilazimika kuyahama makazi yao kwa nguvu duniani kote, wakikimbia migogoro, mateso, majanga ya asili na vitisho vingine. Idadi hiyo imekuwa ikiongezeka.

Clements alisema watu hao wana fursa ndogo za kurejea nyumbani kwa sababu ya kutokuwepo kwa amani. Wakimbizi wengi na watu wasio na makazi "wamekuwa nje ya nyumbani kwao kwa karibu kizazi kimoja, wakati mwingine miongo.” Alisema msaada wa muda mrefu ni "muhimu sana" sio tu kwa wale ambao wanalazimika kukimbia lakini pia jamii zinazowapokea.

Alirejelea hali ya Mashariki ya Kati, ambayo imeshuhudia migogoro kadhaa, kama vile vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Syria na mapigano kati ya Israel na Hamas katika Ukanda wa Gaza, na migogoro mingine, kama vile mgogoro wa Sudan.

Clements alisema shirika hilo lina wasiwasi mkubwa kuhusu "athari inayoenea" kwa mgogoro wa Gaza unaoonekana sasa Mashariki ya Kati. Alisema eneo hilo linahitaji kusaidiwa sana na akaelezea matumaini ya kusitishwa kwa mapigano katika mgogoro huo.

Alisema, "Hali hizi kubwa, ngumu haziwezi kutatuliwa bila mwitikio wa jumuiya ya kimataifa." Aliongeza kuwa ni muhimu kwamba mwitikio hauhusishi serikali tu, bali pia pamoja na wananchi, jamii, na wafanyabiashara kujaribu kutafuta suluhu.