Maswali na Majibu: Cha kufanya maji yanapokatika (3)

(3) Vitu unavyopaswa kwenda navyo kwenye vituo vya kusambazia maji

NHK inajibu maswali yanayohusiana na upunguzaji wa madhara ya majanga. Nchini Japani maji salama ya bomba yapatikana muda wowote. Lakini watu wanakabiliwa na changamoto kubwa pale matetemeko ya ardhi ama majanga mengine yanaposababisha kukatika kwa maji. Katika makala hii, tunakuletea taarifa ya kusaidia kuchukulia kwa utulivu hali ya kukatika kwa maji inapotokea. Leo tutaangazia kile unachopaswa kwenda nacho katika kituo cha dharura cha kusambazia maji.

Kwanza, unapaswa kuandaa dumu lenye uwazi mkubwa wa kujazia maji. Bomba ya maji ya lori la maji ina kipenyo kikubwa kuliko bomba za kawaida, hivyo kwa kutumia dumu lenye uwazi mkubwa, unaweza kujaza maji katika muda mfupi bila ya kumwaga maji.

Kisha unapaswa kufikiria namna ya kupeleka nyumbani dumu lililojaa maji kabla ya kwenda kwenye kituo cha kusambazia maji. Uwingi wa maji unayopata, dumu linakuwa zito zaidi. Ikiwa unalazimika kutembea na maji hadi nyumbani, unashauriwa kutumia begi ya mgongoni ama toroli ili usiumie mgongo wako. Ikiwa utatumia begi ya mgongoni, weka mfuko mkubwa wa plastiki ndani ya begi. Hakikisha unafunga vizuri mwishoni baada ya kuujaza maji. Ikiwa unataka kujihakikishia usalama, tumia mifuko miwili.
Na vituo vipya vya kuingia na gari hadi ndani vimeripotiwa kuibuka hivi karibuni. Unasimamisha gari katika kituo kama hicho ambapo wafanyakazi wanajaza maji kwenye tangi lako.

Pale vituo vya kusambazia maji vinapoanzishwa, kwa kawaida unaweza kuangalia mahali na lini huduma inapatikana katika tovuti za serikali za maeneo husika.
Katika kituo cha kusambazia maji, tafadhali fuata maelekezo ya wafanyakazi katika kituo hicho.

Taarifa hii ni sahihi hadi kufikia Mei 22, 2024.