Urusi yaanza mazoezi ya kijeshi ya silaha za nyuklia

Wizara ya ulinzi ya Urusi imetangaza kuanza kwa mazoezi yanayoigiza kurushwa kwa silaha za kimkakati za nyuklia. Wizara hiyo ilitoa taarifa jana Jumanne ikisema vikosi vyake vinajibu vitisho vya “kichokozi” kutoka mataifa ya Magharibi.

Wizara hiyo ya ulinzi ya Urusi ilitoa picha ya video ya kile inachosema ni hatua ya kwanza ya mazoezi hayo. Ilisema mazoezi hayo yanafanyika katika Wilaya ya Kijeshi ya Kusini, eneo la mpaka ambalo linajumuisha sehemu za Ukraine zilizopo chini ya udhibiti wa Urusi.

Rais Vladimir Putin wa Urusi ameagiza mazoezi hayo kufanyika katika hatua tatu. Aliwaalika wale aliowaita kuwa ni “Wabelarusi wenzake” ili kujiunga katika hatua ya pili ya mazoezi hayo. Nchi ya Belarus imepeleka na kuziweka tayari baadhi ya silaha za nyuklia za Urusi katika eneo lake.

Wizara ya Mambo ya Nje ya Urusi mnamo Mei 6 ilitoa taarifa ikisema mazoezi hayo ni jibu kwa taarifa iliyotolewa na Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron ambapo aliashiria kupeleka wanajeshi wa Ulaya nchini Ukraine. Pia ilimgusia Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza David Cameron akisema wanajeshi wa Ukraine wanaweza kutumia silaha za Uingereza kushambulia eneo la urusi.