Netanyahu apinga ombi la kukamatwa lililotolewa na mwendesha mashtaka wa ICC

Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amepinga vikali uamuzi wa mwendesha mashtaka wa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu, ICC ya kutaka kukamatwa kwa viongozi wa Israel.

Mwendesha mashtaka mkuu wa ICC, Karim Khan, alisema juzi Jumatatu kwamba anaomba hati za kukamatwa kwa watu watano, akiwemo Netanyahu na kiongozi wa Hamas katika Ukanda wa Gaza, Yahya Sinwar.

Katika kujibu, Netanyahu alisema katika ujumbe wa video juzi Jumatatu, "Khan anaunda usawa uliopotoka na wa uongo wa kimaadili kati ya viongozi wa Israel na wafuasi wa Hamas."

Gazeti la Israel la Haaretz liliripoti jana Jumanne kwamba serikali ya Israel "itajaribu kuishawishi serikali ya Marekani na Bunge la Kongresi kuiwekea vikwazo ICC kutokana na ombi la mwendesha mashtaka huyo."