Waziri wa mambo ya nje wa China amlaani raisi mpya wa Taiwan kwa jina

Waziri wa Mambo ya Nje wa China Wang Yi amemlaani moja kwa moja Rais mpya wa Taiwan Lai Ching-te siku moja baada ya kuapishwa kwake.

Wizara ya mambo ya nje ya China inasema Wang alitangaza msimamo wa China kwenye suala la Taiwan katika mkutano wa mawaziri wa mambo ya nje wa Shirika la Ushirikiano wa Shanghai uliofanyika jana Jumanne nchini Kazakhstan.

Wang alinukuliwa akisema kwamba Taiwan ni kiini cha masuala ya misingi ya China na kwamba shughuli za kutafuta uhuru ni vigezo vinavyoharibu zaidi amani katika Mlango Bahari wa Taiwan.

Alimlaani Lai kwa kuisaliti nchi yake na mababu zao na kuviita vitendo vyake kuwa ni vya aibu.

China inamchukulia Lai kama mtu anayetaka kujitenga na mpaka sasa imekataa kufanya mazungumzo naye kwa kuwa amekataa kukubali sera ya China ya “China moja.”