Japani, China na Korea Kusini zinajiandaa kwa mkutano wa viongozi wakuu wiki ijayo

Maandalizi yanaendelea kwa mkutano kati ya viongozi wa Japani, China na Korea Kusini wiki ijayo. Watumishi wa serikali wanalenga kutoa hati kulingana na matokeo ya majadiliano katika maeneo kadhaa.

Mawaziri wakuu wa Japani Kishida Fumio, na China Li Qiang na Rais wa Korea Kusini Yoon Suk-yeol wamepangiwa kukutana jijini Seoul Mei 26 na 27.

Vyanzo vya habari vya serikali ya Japani vinasema viongozi hao wanatarajiwa kushirikishana maoni kwamba ni muhimu kufanya kazi kuelekea amani na uthabiti wa eneo hilo kwa njia inayolenga siku zijazo.

Wanasema mipango inaendelea kwa viongozi hao kuthibitisha kuwa nchi zao zitaongeza ushirikiano katika maeneo yaliyojadiliwa na mawaziri wao wa mambo ya nje mwezi Novemba mwaka jana. Maeneo hayo ni pamoja na uchumi, biashara, mabadilishano ya watu, usalama na afya ya jamii ikiwa ni pamoja na kukabiliana na magonjwa ya kuambukiza.

Watumishi wanafanya kazi kwa bidii kubaini jinsi viongozi hao wataweza kuafikiana juu ya kuanza tena mazungumzo kwa ajili ya makubaliano ya biashara huria ya pande tatu. Mazungumzo kuhusu suala hilo yamekwama tangu mwaka 2019.