Vyama tawala vya Japani vinapanga kukutana na afisa mwandamizi wa China

Maafisa waandamizi wa vyama tawala nchini Japani wiki ijayo wanatarajiwa kukutana na afisa wa ngazi ya juu wa Chama cha Kikomunisti cha China.

Vyanzo vya habari vinasema Liu Jianchao, mkuu wa Idara ya Kimataifa ya Kamati Kuu ya Chama cha Kikomunisti cha China, anapanga kuzuru Japani.Wanasema chama tawala cha Japani cha Liberal Democratic, LDP na mshirika wake mdogo Komeito vilimualika.

Mipango inaendelea kwa mkutano wa Mei 29 kati ya Liu na maafisa wa chama tawala cha Japani, akiwemo Katibu Mkuu wa LDP Motegi Toshimitsu na Mwakilishi Mkuu wa Komeito Yamaguchi Natsuo.

Wanatarajiwa kujadili kuanzishwa tena kwa mikutano ya mashauriano kati ya maafisa waandamizi wa vyama tawala vya nchi hizo mbili.

Maafisa hao walikuwa wakifanya mkutano mara moja kwa mwaka, lakini hawajakutana tangu mwaka 2018.