Ukraine yaonya juu ya kampeni ya taarifa za upotoshaji ya Urusi inayomlenga Zelenskyy

Serikali ya Ukraine imetoa wito kwa watu kuchukua tahadhari dhidi ya taarifa za upotoshaji za Urusi zinazotilia shaka uhalali wa urais wa Volodymyr Zelenskyy.

Muhula wa miaka mitano wa Zelenskyy kama rais ulitakiwa kumalizika jana Jumatatu, lakini bado yupo madarakani. Uchaguzi wa urais, uliopangwa kufanyika mwezi Machi, haukufanyika kutokana na sheria ya kijeshi iliyowekwa baada ya Urusi kuanza uvamizi wake nchini Ukraine.

Idara ya Ujasusi wa Kigeni ya Urusi katika taarifa jana Jumatatu ilisema kwamba uungwaji mkono wa Zelenskyy kutoka kwa raia wa Ukraine unapungua. Idara hiyo ilisema Zelenskyy alihisi kuwa wadhifa wake ulikuwa hatarini, na kwamba alijaribu kwa hali na mali kumwondoa yeyote ambaye hawezi akamtegemea kabla ya kumalizika kwa muhula wake.

Serikali ya Rais wa Urusi Vladimir Putin imehoji uhalali wa kisiasa wa Rais Zelenskyy. Lakini kura ya maoni iliyofanywa mwezi Februari na Taasisi ya Kimataifa ya Sosiolojia ya Kyiv ambayo ni kampuni ya utafiti wa maoni ya umma nchini Ukraine, ilibaini kwamba asilimia 69 ya raia wanadhani Zelenskyy anapaswa kusalia madarakani hadi sheria ya kijeshi iondolewe.

Kituo cha Kupambana na Taarifa za Upotoshaji nchini Ukraine jana Jumatatu kilitoa wito wa kuchukuliwa kwa tahadhari dhidi ya taarifa za uongo zinazoenezwa na Urusi. Kilisema Urusi inatumai kuchochea janga la kisiasa ili kudhoofisha usaidizi wa kimataifa kwa Ukraine na pia kudhoofisha uwezo wake wa ulinzi.