Japani kutuma msaada wa kibinadamu Gaza kupitia UNRWA

Serikali ya Japani itatuma kundi la bidhaa za msaada wa kibinadamu katika Ukanda wa Gaza kupitia kwa Shirika la Umoja wa Mataifa linalowahudumia Wakimbizi Wakipalestina, UNRWA.

Maafisa wa Japani wamekabidhi orodha ya bidhaa za msaada kwa maafisa wa shirika hilo wakati wa hafla iliyoandaliwa jijini Cairo nchini Misri. Hafla hiyo ilihudhuriwa na Balozi wa Japani nchini Misri Oka Hiroshi na mkuu wa ofisi ya mwakilishi wa UNRWA jijini Cairo, Sahar Al-Jobury.

Serikali ya Japani inajiandaa kutuma mablanketi 5,000, vyombo vya maji 10,000 na bidhaa zingine kufuatia ombi la UNRWA.

Serikali ya Japani ilisitisha ufadhili kwa shirika hilo kufuatia tuhuma kwamba baadhi ya wafanyakazi wa UNRWA walihusika katika shambulizi la Hamas nchini Israel mwezi Oktoba mwaka jana.

Hata hivyo, Japani ilitangaza kuwa itarejesha usaidizi wake wa kifedha kutokana na kuimarika kwa uongozi wa shirika hilo.

Katika hafla hiyo, Oka alisema nchi nyingi zinarejesha usaidizi wao ili kusaidia kuboresha hali ya kibinadamu katika eneo la Gaza. Aliongeza kuwa kufikisha bidhaa za msaada kutoka Japani hadi kwa mikono ya watu wenye uhitaji ni muhimu.

Sahar Al-Jobury alisema UNRWA ni shirika pekee kwa Wapalestina na ni nembo kwao. Aliongeza kuwa ni jukumu la pamoja la jumuiya ya kimataifa kuendelea kufadhili UNRWA, na kamwe shirika hilo halipaswi kutelekezwa tena.