Waziri Mkuu wa Japani atuma salamu za rambirambi kufuatia kifo cha Raisi

Waziri Mkuu wa Japani Kishida Fumio katika taarifa iliyotolewa jana Jumatatu ametuma salamu zake za rambirambi kufuatia kifo cha Rais wa Iran Ebrahim Raisi.

Katika taarifa hiyo, Kishida amesema amehuzunishwa mno na kifo cha ghafla cha Rais Raisi.

Amesema alikuwa na mfululizo wa majadiliano ya wazi juu ya uhusiano wa pande mbili na hali katika eneo hilo kutokana na uhusiano wa kirafiki wa muda mrefu baina ya nchi zao.

Kishida aliongeza kuwa kwa niaba ya serikali na watu wa Japani, angependa kutoa salamu zake za dhati za rambirambi kwa serikali na watu wa Iran na familia ya Rais Raisi.

Kishida alikutana na Raisi jijini New York nchini Marekani mwaka jana na mwaka 2022. Pia alizungumza naye kwa njia ya simu mara mbili.