Maswali na Majibu: Cha kufanya maji yanapokatika (1)

(1) Kufunga vali kuu ya maji

NHK inajibu maswali kuhusiana na ukabilianaji wa majanga. Nchini Japani maji salama ya bomba yanapatikana wakati wowote. Lakini watu wanakabiliwa na usumbufu mkubwa wakati matetemeko ya ardhi au majanga mengine yanaposababisha kukatika kwa maji. Katika mfululizo huu, tunakuletea taarifa ya kukusaidia kukabiliana kwa utulivu maji yanapokatika. Katika sehemu ya kwanza, tunaangazia kufunga vali za maji.

Hatua ya kwanza unayopaswa kuchukua wakati maji yanapokatika ni kufunga vali kuu ya maji. Hii itasaidia kuzuia maji ya tope kuingia kwenye mabomba ya maji ya ndani kwako. Katika majanga yaliyopita, kulikuwa na visa vya maji ya tope kusababisha vyoo na mifumo ya kupasha maji kutofanya kazi.

Kwenye nyumba, vali hiyo ipo ndani ya sanduku la mita ya maji chini ya ardhi ya nyumba husika. Kifuniko cha mraba cha chuma au plastiki kipo juu ya ardhi.

Katika majengo yenye fleti nyingi, mita za maji zinaweza kuwekwa tofauti kwa nyumba za jumuiya au fleti. Kwa nyumba za jumuiya, mita mara nyingi huwa ndani ya sehemu isiyo wazi kando ya mlango wa kila chumba.

Katika fleti, mita zinaweza kuwa chini ya ardhi kama nyumba za kawaida au zinaweza kuwa kwenye ushoroba au sehemu nyingine ya wazi. Mita za kaya zingine huenda zikawekwa katika eneo kama hilo, hivyo angalia namba ya chumba katika mita kuhakikisha unafunga vali ya chumba chako mwenyewe.

Zungusha vali kuelekea upande wa kulia ili kufunga maji, peleka upande wa kushoto ili kurejesha maji. Ili kuwa salama, pia ni bora kufunga vali za choo, mfumo wa kupasha maji na mashine ya kufulia nguo.

Taarifa hii ni sahihi hadi kufikia Mei 20, 2024.