Maafisa wa Ukraine: Mashambulizi ya Urusi yaua watu 10 katika eneo la Kharkiv

Mamlaka katika eneo la mashariki mwa Ukraine la Kharkiv zinasema kuwa mashambulizi ya Urusi yamesababisha vifo vya watu 10 na kuwajeruhi wengine 25.

Jana Jumapili gavana wa Kharkiv alisema kwamba raia watano waliuawa na tisa kujeruhiwa wakati vijiji viwili viliposhambuliwa kwa roketi nyingi.

Meya wa jiji la Kharkiv alisema kwamba siku hiyo hiyo makombora mawili ya Urusi yalishambulia kituo cha burudani katika kiunga cha jiji hilo, na kuua watu watano na kujeruhi 16.

Kufuatia mashambulizi hayo, Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskyy aliandika kwenye mtandao wa kijamii, "Dunia inaweza kukomesha ugaidi wa Urusi." Alizisihi Marekani na nchi za Ulaya kutoa msaada wa mifumo ya ziada ya ulinzi wa anga kwa eneo la Kharkiv.