Watu wasiopungua 66 wafariki kwa mafuriko katika jimbo la Faryab kaskazini mwa Afghanistan

Mamlaka za Afghanistan zimesema mafuriko katika jimbo la kaskazini la Faryab yamesababisha vifo vya watu wasiopungua 66.

Mamlaka za jimbo hilo zimesema mafuriko hayo ya juzi Jumamosi pia yamesomba na kuharibu nyumba karibu 1,500 na watu wanane hawajulikani walipo. Shughuli za uokoaji zinaendelea katika eneo hilo.

Afghanistan imekuwa ikikumbwa na mfululizo wa mafuriko kutokana na mvua kubwa mwezi huu. Watu wasiopungua 180 wamethibitishwa kufariki katika jimbo la Baghlan na majimbo mengine kaskazini mwa nchi hiyo, wakati watu wasiopungua 50 wamepoteza maisha katika jimbo la katikati mwa nchi hiyo la Ghor.

Changamoto kubwa kwa Afghanistan ni kutoa msaada kwa walioathiriwa na mafuriko hayo, na kurejesha maisha yao ya kawaida. Nchi hiyo inakabiliwa na uchumi mgumu pamoja na uhaba wa chakula, chini ya utawala wa Taliban iliyotwaa tena madaraka miaka mitatu iliyopita.