Sullivan akutana na Netanyahu nchini Israel kuhusiana na hali ya Rafah

Mshauri wa Usalama wa Taifa wa Ikulu ya Marekani Jake Sullivan jana Jumapili amekutana na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu nchini Israel kujadili operesheni za kijeshi mjini Rafah kusini mwa Ukanda wa Gaza.

Ikulu ya Marekani imesema kuwa “pande hizo mbili zimejadili njia za kuhakikisha Hamas inashindwa huku zikipunguza madhara kwa raia.”

Sullivan ameripotiwa kusisitiza msimamo wa muda mrefu wa Rais Joe Biden juu ya Rafah.

Anaaminika kusisitiza tena msimamo wa Marekani wa kupinga mashambulizi makubwa ya ardhini mjini Rafah ambayo yanaweza kusababisha vifo vya raia.

Shirika la Umoja wa Mataifa linalohudumia wakimbizi Wapalestina, UNRWA, limesema watu wapatao 800,000 wamelazimika kukimbia Rafah, na kwamba wahamaji hao hawana maji salama.