Ripoti: Mafuriko katikati mwa Afghanistan yaua watu wasiopungua 50

Mamlaka za Afghanistan zimeripotiwa kusema kwamba mafuriko ya hivi karibuni nchini humo yameua watu wasiopungua 50 na kuharibu maelfu ya nyumba.

Shirika la habari la Reuters na vyombo vya habari vya nchi hiyo vilizinukuu mamlaka hizo jana Jumamosi zikisema mvua kubwa iliyoanza kunyesha juzi Ijumaa zilisababisha mafuriko kwenye jimbo la katikati ya nchi hiyo la Ghor.

Picha za video kutoka kwenye ukanda wa janga zinaonesha maji ya mafuriko yaliyofunika barabara na maduka yaliyojaa bidhaa yakiwa yamefunikwa na matope.

Vyombo vya habari vya nchi hiyo vinasema mvua zaidi inatarajiwa leo Jumapili huko Ghor na majimbo mengine 15, kuongeza wasiwasi juu ya uharibifu zaidi.

Kipindi cha juma moja lililopita tu, jimbo la Baghlan na mengineyo huko kaskazini mwa nchi hiyo yalikumbwa na mafuriko.

Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Masuala ya Binadamu ilisema mafuriko hayo yamesababisha vifo vya watu 180.