Ukraine yaimarisha sheria ya uhamasishaji watu kuingia jeshini ili kuondokana na uhaba wa wanajeshi

Ukraine imeimarisha sheria yake ya uhamasishaji jeshini ili kushughulikia uhaba mkubwa wa wanajeshi.

Kufuatia uvamizi wa Urusi, wanaume raia wa Ukraine wenye umri wa miaka 18 hadi sitini wamekatazwa kuondoka nchini humo.

Sheria hiyo ambayo ilianza kazi jana Jumamosi inasema kwamba wanaume waliopo katika umri huo hivi sasa ni lazima waandikishwe anuani zao na taarifa zingine binafsi na jeshi ndani ya siku sitini.

Hatua hiyo ina lengo la kuzuia ukwepaji wa kuingia jeshini na inakuja baada ya Ukraine kupunguza umri wa uhamasishaji kuingia jeshini kutoka miaka 27 hadi 25.

Chombo huru cha habari kilifanya utafiti mwezi Januari na Februari kikiwauliza wanaume raia wa Ukraine kati ya umri wa miaka 18 na 55.

Asilimia 18 ya waliojibu walisema sheria hiyo haina umuhimu, huku asilimia zaidi ya 80 walisema sheria hiyo ni muhimu lakini lazima ifanyike kwa usawa.

Asilimia zaidi ya 30 walisema walikuwa tayari kwenda jeshini ikiwa wataitwa, lakini takribani nusu walisema hawako tayari. Katika kipindi hiki cha hali ya wasiwasi, watu bado wanajaribu kuondoka Ukraine kinyume cha sheria ili kukimbia kuitwa kujiunga na jeshi.

Majaribio mengi ya kukimbia nchi kuelekea mataifa jirani yamekuwa yakifanywa na madalali chini ya masharti magumu. Baadhi ya watu wamepoteza maisha yao wakijaribu kuvuka mto na kupita milima mikubwa.

Redio ya Free Europe ilimnukuu polisi wa mpaka wa Romania akisema kwamba wanaume raia wa Ukraine wapatao 11,000 wa umri wa kuingia jeshini wameingia kinyume cha sheria nchini Romania tangu kuanza kwa uvamizi wa Urusi.