Viongozi wa dunia wanalaani ‘kuongezeka kwa maumivu’ katika ukanda wa Gaza

Viongozi wa dunia wanaendelea kuelezea tahadhari juu ya kuongezeko kwa jeshi la Israel katika eneo la Rafah. Wameelezea "wasiwasi wao mkubwa" juu ya matokeo ya janga la kibinadamu. Lakini Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu ameahidi kushikamana na operesheni hiyo na kuendelea na kampeni ya "kuelekea ushindi.”

Netanyahu alifanya ziara ya anga katika ukanda wa Gaza juzi Alhamisi na kupokea taarifa kutoka kwa makamanda. Aliviambia vikosi vyake kwenye kambi ya Bnei Netzarim nchini Israel kwamba ushindi ni muhimu kuondoa “njia za usafirishaji” inayotumiwa na wapiganaji wa Hamas.

Netanyahu alisema, “Vita hii, ambayo ninyi ni wahusika muhimu, ni vita itakayoamua mambo mengi katika mapigano haya.”

Jana Ijumaa, Vikosi vya Ulinzi vya Israel vilisema vimeipata miili ya mateka watatu waliouawa wakijaribu kutoroka shambulio la Hamas kwenye tamasha la muziki Oktoba 7, na baadaye kupelekwa Gaza.

Nchi wanachama wa Umoja wa Nchi za Kiarabu zilifanya mkutano wa viongozi wakuu juzi Alhamisi na kuwashutumu viongozi wa Israel kwa kuzuia juhudi za kusitisha mapigano na kuzidisha vitendo vyao vya kichokozi.

Katibu Mkuu wa Umioja wa Mataifa Antonio Guterres alihutubia mkutano huo na kuwaambia viongozi kuwa hakuna kinachoweza kuhalalisha kile alichokiita “adhabu ya pamoja” kwa watu wa Palestina.