Korea Kaskazini yasema ilifanya jaribio la kimkakati la kombora la balistiki

Korea Kaskazini imetangaza kuwa jana Ijumaa ilifanya jaribio la kimkakati la kombora la balistiki lililohusisha mfumo mpya wa kujitegemea unaojiendesha.

Kituo cha habari cha taifa cha Korean Central Television kilisema leo Jumamosi kwamba Mamlaka ya Makombora ya nchi hiyo ilifanya jaribio la urushaji kwenye maji nje ya pwani ya mashariki ya Rasi ya Korea. Ripoti hiyo ilisema kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong Un alishuhudia. Picha iliyotolewa inaonyesha kombora likiripotiwa likipiga shabaha yake.

Korea Kaskazini imekuwa ikiendeleza makombora ya kimkakati ya balistiki, ambayo nchi hiyo inasema yanalenga kubeba vichwa vya nyuklia. Waangalizi wanasema makombora hayo yanaweza kutumiwa katika mashambulizi yanayoweza kutokea kwenye kambi za kijeshi za Korea Kusini na Marekani zilizopo nchini Korea Kusini.