Maswali na Majibu: Usijihusishe na kazi za vibarua za udangayifu (5)

(5) Mawakala wa mauzo mtandaoni

NHK inajibu maswali kuhusu kuhakikisha usalama katika maisha ya kila siku. Kumekuwepo na mfululizo wa visa ambapo raia wa kigeni nchini Japani wanajihusisha na uhalifu baada ya kutuma maombi ya “kazi nyepesi zenye malipo ya juu” zinazopachikwa katika mitandao ya kijamii. Katika mfululizo huu, tutatoa mifano ya kile kinachoitwa kazi za vibarua za udanganyifu ambazo kamwe haupaswi kukubali kuzifanya. Leo hii, tunaangazia mawakala wa mauzo mtandaoni.

Polisi wanaripoti ongezeko la idadi ya visa ambayo vinajaribu kuwashawishi raia wa kigeni kufanya kazi za udanganyifu kupitia mitandao ya kijamii kwa kutumia misemo kama vile, “malipo ya juu kwa kuuza tu bidhaa mtandaoni”, au “utalipwa tu kwa kutoa akaunti yako ya mtandao wa gulio.” Kazi za udanganyifu kama hizo ambazo zinahusisha kuuza bidhaa zenye chapa bandia au bidhaa ambazo zimepatwa kwa njia isiyokuwa halali ni vitendo vya uhalifu.

Mwezi Agosti mwaka 2023, polisi mkoani Osaka walimkamata mwanamume Mchina kwa tuhuma za kukiuka Sheria ya Vifaa vya Dawa na Tiba. Mwanamume huyo mwenye umri wa miaka ya 30 alikuwa amehifadhi chupa 148 za vipodozi bandia vya chapa maarufu kwa ajili ya mauzo. Polisi wanasema mwanamume huyo ni sehemu ya kundi la uhalifu linalouza vipodozi bandia. Kundi hilo lilibainika kukusanya watu kupachika au kuwasilisha bidhaa hizo kupitia mtandao wa kijamii wa China. Polisi pia wamewakamata wanaume wengine wawili kwa tuhuma za kuuza bidhaa bandia.

Unapaswa kuchukua tahadhari ya kutoshawishiwa kupitia misemo ya udanganyifu kama vile “pesa rahisi” au “si kinyume cha sheria.” Hakikisha unawasiliana na polisi ikiwa utajipata matatani au una mashaka yoyote.

Taarifa hii ni sahihi hadi kufikia Mei 17, 2024.