Rais Zelenskyy wa Ukraine: Hali mjini Kharkiv ‘ni ngumu zaidi’

Vikosi vya Ukraine vimekuwa vikihangaika kulinda maeneo yaliyopo karibu na mji wao wa pili kwa ukubwa zaidi wa Kharkiv. Rais Volodymyr Zelenskyy alielekea mjini humo jana Alhamisi kukutana na makamanda na kujadili namna wanavyoweza kuimarisha vikosi vyao.

Zelenskyy ameahirisha safari zote za nje ya nchi ili kuangazia hali ambayo anasema ni “ngumu zaidi.” Amesema vikosi vyake vinawasababishia Warusi “hasara kubwa” lakini vinahitaji kwa dharura mifumo ya ulinzi ya anga hasa ile ya Patriots iliyotengenezwa nchini Marekani.

Bado, kwa mara nyingine, anatoa wito kwa “majirani wa Ukraine na Ulaya yote” kufanya kazi pamoja ili kukabiliana na tishio hilo.

Makamanda wa Umoja wa Kujihami wa Nchi za Kaskazini mwa Atlantiki, NATO wanasema usaidizi zaidi upo njiani. Wakati wakiwahutubia wanahabari mjini Brussels nchini Ubelgiji, walisema wameshawishika kwamba kutakuwa na “maboresho ya dhati” kiasi katika silaha ambazo Ukraine itapokea hivi karibuni.