China inaripotiwa kusitisha usajili wa makampuni ya usafirishaji wa vyakula vya baharini kutoka Japani

NHK imebaini kuwa mamlaka za China zimesitisha usajili wa vituo vinavyotumiwa na wasafirishaji wa vyakula vya baharini kutoka Japani.

Makampuni ya Kijapani yanayotaka kusafirisha bidhaa za baharini kwenda China yanalazimika kusajili usindikaji, kuhifadhi na vituo vingine nchini Japani na mamlaka ya forodha ya China.

Mwezi Agosti mwaka jana, mamlaka za China zilisitisha uagizaji wa vyakula vya baharini vya Japani, kufuatia kumwagwa baharini kwa maji yaliyotibiwa na kuzimuliwa kutoka mtambo wa nyuklia wa Fukushima Namba Moja ulioharibiwa.

Vyanzo vinavyofahamu suala hilo vinasema usajili wa vituo vya wauzaji bidhaa za nje ulitumika hadi mwezi uliopita.

Vyanzo vingine vya karibu na serikali ya Japani vinasema mamlaka ya China ilisimamisha usajili wote mwezi huu.

Wanasema upande wa China haujatoa maelezo yoyote kwa Japani kuhusu hatua ya hivi karibuni.

Haya yanajiri huku serikali zikifanya mazungumzo kuhusu kumwagwa kwa maji yaliyotibiwa na kuzimuliwa mwaka huu.

Vyanzo vya serikali ya Japani vinasema wanahitaji kujua ni kwa nini China ilichagua wakati huu kusitisha usajili.