Putin na Xi wasaini taarifa ya pamoja inayojumuisha ukuzaji zaidi wa ushirikiano wa kijeshi

Marais Vladimir Putin wa Urusi na Xi Jinping wa China wamesaini taarifa ya pamoja inayojumuisha mipango ya kukuza zaidi ushirikiano wa kijeshi wa pande mbili.

Putin na Xi walifanya mazungumzo jana Alhamisi jijini Beijing wakati wa ziara rasmi ya Putin nchini China. Hiyo ni ziara ya kwanza ya Putin nje ya nchi tangu alipoanza muhula wake wa tano mapema mwezi huu.

Katika taarifa hiyo, Urusi inaipongeza China kwa utayari wake wa kutekeleza jukumu muhimu katika kufikiwa azimio la kisiasa na kidiplomasia katika mzozo wa Ukraine.

Taarifa hiyo pia inajumuisha mipango ya kupanua wigo wa mazoezi ya pamoja ya kijeshi baina ya Urusi na China kama sehemu ya kuimarisha zaidi ushirikiano wao wa kijeshi.

Viongozi hao wawili baadaye walifanya mazungumzo yasiyo rasmi.

Nchi hizo mbili zimeripotiwa kufanya mazungumzo yasiyo rasmi kwa zaidi ya saa nne. Hatua hiyo inaashiria kuwa zinaimarisha uhusiano wa pande mbili huku zikiangazia mataifa ya Magharibi, ambayo yametofautiana na Urusi na China kuhusu hali nchini Ukraine na Asia Mashariki.