Afisa wa UN anayesimamia masuala ya wanawake aushutumu mgogoro wa Gaza akiutaja kuwa ‘vita dhidi ya wanawake’

Afisa mwandamizi wa Shirika la Wanawake la Umoja wa Mataifa la UN Women linalounga mkono kuboreshwa kwa haki za wanawake na wasichana kote duniani, ameshutumu mapigano yanayoendelea katika Ukanda wa Gaza akiyataja kuwa “vita dhidi ya wanawake.”

Kirsi Madi ni Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa UN Women anayeshughulikia Usimamizi wa Rasilimali, Uendelevu na Ushirikiano. Alizungumza na NHK jijini Tokyo jana Alhamisi.

Alibainisha kwamba zaidi ya wanawake 10,000 wenye umri wa miaka 18 ama zaidi wamefariki katika kipindi cha zaidi ya miezi sita ya mapigano hayo. Alisema 6,000 kati yao walikuwa ni kina mama na watoto 19,000 kwa sasa wanaaminika kupoteza mama zao.

Aliongeza kuwa, “Athari za vita kwa watoto, wanawake na wasichana hasa zinatisha kwa kweli,” na kuonya kwamba hakuna mmoja wao ambaye yuko salama katika eneo la Gaza hii leo.

Pia alielezea wasiwasi wake kuhusu namna usambazaji wa misaada katika eneo hilo umepungua kasi baada ya Israel kuchukua udhibiti wa mpaka wa Rafah. Ametoa wito wa mapigano katika eneo la Gaza kusitishwa mara moja na ufikaji usiozuiliwa wa binadamu katika ukanda huo.