Marekani yasema imeweka gati la muda la kuwasilisha msaada eneo la Gaza

Jeshi la Marekani linasema limeweka gati la muda la kuwasilisha bidhaa za msaada katika Ukanda wa Gaza. Hali ya kibinadamu katika ukanda huo inasalia mbaya kufuatia mapigano kati ya Israel na kundi la Hamas.

Kamandi Kuu ya Marekani ilisema jana Alhamisi kuwa maafisa wake waliweka gati hilo kwenye ufukwe wa Gaza majira ya saa 1:40 asubuhi kwa saa za eneo hilo. Imesema hakuna wanajeshi wa Marekani walioingia eneo la Gaza kama sehemu ya juhudi hizo.

Iliongeza kuwa malori yaliyobeba msaada wa kibinadamu yalitarajiwa kuanza safari kuelekea ufukwe huo siku chache zijazo. Umoja wa Mataifa utapokea msaada huo na kuratibu usambazaji wake.

Rais wa Marekani Joe Biden alisema wakati akitoa hotuba kwa taifa mwezi Machi mwaka huu kwamba gati hilo litawezesha kiwango cha msaada wa binadamu unaosafirishwa kuelekea eneo la Gaza kila siku kuongezwa kwa kiasi kikubwa.

Lakini runinga ya CNN iliripoti juma lililopita kuwa hali mbaya ya hewa na bahari huenda ikazuia kwa kiasi kikubwa uwezo wa magati kutumia yanayoelea hata pale yatakapoanza kufanya kazi.