Maswali na Majibu (97) Usijihusishe na kazi za vibarua za udanganyifu (4)

(4) Mawakala wa ununuzi

NHK inajibu maswali kuhusu kuhakikisha usalama katika maisha ya kila siku. Kumekuwepo na mfululizo wa visa ambapo raia wa kigeni nchini Japani wanajihusisha na uhalifu baada ya kuomba “kazi nyepesi zenye malipo makubwa” zinazotumwa kwenye mitandao ya kijamii. Katika mfululizo huu, tutakujulisha mifano ya kazi zinazoitwa vibarua vya udanganyifu ambazo haupaswi kuzifanya. Leo hii, tunaangazia mawakala wa ununuzi.

Idara ya Polisi ya jiji la Tokyo imeripoti visa ambapo wakazi raia wa kigeni hushawishiwa na marafiki wanaowaahidi malipo makubwa kwa kufanya manunuzi tu kwa niaba yao, na kujikuta wanakuwa washirika wa uhalifu. Katika kisa kimoja, mwanamume Mchina mwenye miaka ya ishirini alikamatwa kwa mashtaka ya ulaghai katika duka la vipodozi jijini Tokyo kwa kuiba kimiminika cha urembo na bidhaa zingine zenye thamani ya yeni 130,000 (takribani dola 830) kwa kutumia njia ya manunuzi isiyoruhusiwa ya pointi za malipo kutoka kwenye programu inayoendeshwa na kampuni ya reli mnamo Juni 2022.

Polisi wanasema mwanamume huyo alifuatwa na mwanamume mwingine Mchina kwenye ukumbi wa karaoke, aliyempatia “kazi rahisi ya kibarua cha uwakala wa ununuzi.” Mshukiwa wa udanganyifu huo anatuhumiwa kutumia utambulisho na nywila ya mtu mwingine iliyopewa na kundi hilo la uhalifu ili kuingia kwenye tovuti na kufanya manunuzi kwa kutumia pointi. Mtu huyo inasemekana alilipwa yeni 40,000 (karibu dola 260) na kundi hilo la uhalifu kama malipo ya manunuzi hayo kwa njia ya udanganyifu. Polisi walibaini kwamba raia wengi wa China wanajihusisha na kazi kama hizo za vibarua, ambapo waombaji mara kwa mara wanashawishiwa kupitia mitandao ya kijamii na kwa mdomo. Polisi wanaonya watu kutojibu ofa za kazi wanazozitilia mashaka kwa sababau tu zimetolewa na mtu fulani wanayemfahamu kutoka nchi wanayotokea ama kwa sababu marafiki zao wanazifanya.

Taarifa hii ni sahihi kuanzia Mei 16, 2024.