Hali ya dharura yatangazwa New Caledonia

Serikali ya Ufaransa, jana Jumatano imetangaza hali ya dharura kwenye eneo lake la New Caledonia huko Pasifiki, kufuatia machafuko makubwa yanayoendelea kwenye eneo hilo.

Machafuko hayo yalizuka Jumatatu jioni kwenye jiji kuu la Noumea na maeneo ya jirani.

Inaonekana machafuko hayo yalitokana na mjadala kwenye bunge la Ufaransa wa kutoa haki ya kupiga kura katika chaguzi za maeneo kwa wakazi zaidi wa New Caledonia. Hatua hii ilizua upinzani kutoka kwa wakazi wa visiwa hivyo wanaotafuta kupata uhuru kutoka kwa Ufaransa.

Serikali ya Ufaransa inasema machafuko hayo yamesababisha vifo vya watu wanne.

Shirika la habari la Reuters limeripoti kuwa mamia ya watu wamejeruhiwa na wengine wasiopungua 80 wamekamatwa.

Uwanja wa ndege wa kimataifa umefungwa tangu Jumatatu.

Serikali ya Ufaransa inasema hii ni mara ya kwanza kwa hali ya dharura kutangazwa kwenye eneo hilo tangu harakati za kudai uhuru zilipoanza kushika kasi mwaka 1985.

Imepanga kupeleka maafisa zaidi wa usalama kusaidia kudhibiti machafuko hayo.