Netanyahu: Operesheni ya Rafah itakamilika ‘katika kipindi cha wiki chache’

Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu anasema mashambulizi ya kijeshi huko Rafah yatadumu "muda wa wiki, sio miezi, sio miaka," akisisitiza haja ya kuangamiza vikosi vinne vya Hamas katika mji huo wa kusini mwa Gaza.

Kituo cha habari cha Marekani, CNBC kilimhoji Netanyahu jana Jumatano.

Waziri mkuu huyo alibainisha kuwa Marekani na Israel “hazijakubaliana.” Lakini alisema, "Wakati mwingine, lazima tu ufanye kile kinachohitajika ili kuhakikisha uhai wako na mustakabali wako."

Vyombo vya habari vinaripoti kwamba Mshauri wa Usalama wa Kitaifa wa Ikulu ya Marekani Jake Sullivan anapanga kusafiri wikiendi hii kutafuta mwanya wa kusitisha mapigano.

Jana Jumatano jeshi la Israel lilisema kwamba lilifanya mashambulizi ya anga kwa takriban shabaha 80 katika eneo la Gaza siku iliyotangulia. Pia jeshi hilo lilisema vikosi vyake vya ardhini "vimeangamiza" idadi kubwa ya wapiganaji wa Hamas huko Rafah na mji wa kaskazini wa Jabalia.

Al Jazeera ilisema takriban watu 10 waliuawa baada ya makombora kuipiga kliniki inayoendeshwa na shirika la Umoja wa Mataifa, UN kaskazini mwa Gaza. Pia iliripoti vifo vingi katika shambulio la katikati mwa jiji, ambapo raia walikuwa wamekusanyika kupata intaneti.