Putin awasili Beijing kwa ajili ya mkutano na Xi

Rais wa Urusi Vladimir Putin amewasili nchini China kwa ajili ya ziara rasmi ya siku mbili. Ni ziara yake ya kwanza nje ya nchi tangu aingie madarakani muhula wake wa tano.

Ndege ya rais iliyombeba Putin ilitua jijini Beijing mapema leo Alhamisi asubuhi. Alipokelewa na maafisa wa China aliposhuka kwenye ndege hiyo.

Ofisi ya rais wa Urusi inasema Putin anafanya mkutano na Rais wa China Xi Jinping, katika jiji hilo, na viongozi hao wawili watatia saini nyaraka za pamoja.

Waangalizi wa mambo wanasema Putin analenga kupata uelewa wa China juu ya msimamo wa Urusi katika hali ya Ukraine huku wakithibitisha mshikamano kati ya pande hizo mbili wanapoongeza msimamo wao wa kukabiliana na nchi za Magharibi.