Waziri Mkuu Mpya wa Singapore aapishwa ili kuchukua nafasi ya Lee anayeondoka

Waziri mkuu wa muda mrefu wa Singapore, Lee Hsien Loong, amejiuzulu na nafasi yake imechukuliwa na naibu kiongozi, Lawrence Wong.

Wong aliapishwa jana Jumatano. Katika hotuba yake ya uapisho, alisisitiza kuwa mabadiliko ya kizazi yamefanyika.

Alitoa wito wa umoja wa kitaifa huku akiwaomba raia wenzake wa Singapore kuungana naye na timu yake na safari yao ya kusonga mbele.

Waziri mkuu huyo mpya, mrasimu wa zamani, ana umri wa miaka 51 na alikulia katika familia ya uchumi wa kati.

Amemrithi Lee, mtoto mkubwa wa waziri mkuu wa kwanza na baba mwanzilishi wa nchi hiyo hayati, Lee Kuan Yew.

Waziri mkuu anayeondoka atahudumu katika baraza la mawaziri la Wong kama waziri mwandamizi.

Uapisho wa Wong unakuja wakati Singapore ikikabiliwa na changamoto zinazokua za ndani na kimataifa. Nadhari inaangaziwa jinsi Wong atakavyoongoza nchi huku kukiwa na kupungua kwa kiwango cha watoto wanaozaliwa na mivutano kati ya Marekani na China.