Waziri Mkuu wa Slovakia apelekwa hospitalini baada ya kupigwa risasi

Waziri Mkuu wa Slovakia Robert Fico amefikishwa hospitalini baada ya kupigwa risasi.

Shirika la habari la Reuters liliripoti kwamba ofisi ya serikali ya Slovakia ilisema Fico yupo katika hali inayotishia uhai wake.

Shambulio hilo lilitokea Handlova katikati mwa Slovakia, ambako Fico alikuwa anahudhuria mkutano wa serikali jana Jumatano.

Shirika la habari la Uingereza BBC lilivinukuu vyombo vya habari vya Slovakia vikiripoti kwamba Fico alishambuliwa kwa risasi alipokuwa akisalimia umati wa watu baada ya mkutano.

Imeripotiwa kwamba Fico amejeruhiwa tumboni na alisafirishwa kwa helikopta kwenda hospitalini.

Mshukiwa wa shambulio hilo ameripotiwa kukamatwa.

Fico alitwaa madaraka kufuatia ushindi wa chama chake cha upinzani kwenye uchaguzi wa bunge mwezi Septemba mwaka jana. Alisihi kusitishwa kwa msaada wa kijeshi kwa Ukraine.