Mwanaharakati wa mageuzi ya ufalme wa Thailand aliyefungwa jela afariki baada ya kugoma kula

Mwanaharakati wa Thailand aliyetaka sheria ya kukashifu ufalme ifanyiwe marekebisho amefariki baada ya mgomo wa kula kwa miezi kadhaa akiwa gerezani.

Netiporn Sanesangkhom, ambaye alikuwa na umri wa miaka 28, alifunguliwa mashtaka na kufungwa mwaka 2022 kwa kutukana ufalme. Alikuwa amefanya kura ya maoni ya umma kuhusu desturi ya kufunga barabara ili magari ya kifalme yapite.

Wanasheria wa Netiporn wanasema alianza mgomo wa kula mnamo mwezi Januari. Wanasema alihamishiwa hospitali ya nje kwa muda mfupi baada ya kuugua, lakini alirudishwa gerezani mwezi uliopita.

Mamlaka ya Thailand inasema Netiporn alikuwa akipokea chakula tangu mwezi Aprili, lakini hali yake ilizidi kuwa mbaya jana Jumanne. Wanaripoti kwamba alithibitishwa kufariki hospitalini.

Mnamo mwaka 2020, mikutano ya hadhara inayotaka marekebisho ya kifalme na mapitio ya sheria ya kukashifu ufalme ilienea nchini Thailand na kuendelea hadi mwaka uliofuata.

Lakini maandamano hayo yalififia baada ya mamlaka kuyakandamiza. Hakuna maandamano yoyote ya kupinga ufalme yanayofanyika sasa.