Mtafiti wa China mwenye makao yake nchini Japani ahukumiwa kifungo cha miaka 6 jela nchini China

Mwanazuoni raia wa China aliyefunguliwa mashtaka ya kufanya ujasusi nchini Japani amehukumiwa kifungo cha miaka sita jela nchini China.

Yuan Keqin, profesa mstaafu katika Chuo Kikuu cha Elimu cha Hokkaido nchini Japani, alikamatwa Mei mwaka 2019, alipokuwa nchini mwake akikaa kwa muda. Baadaye alifunguliwa mashtaka ya kuhusika na ujasusi wa muda mrefu kwa ombi la idara ya intelijensia ya Japani.

Vyanzo vya habari vilivyopo karibu na Yuan vilisema alipokea hukumu hiyo mwezi Januari katika mahakama ya Changchun, katika jimbo la Jilin kaskazini mashariki mwa China.

Yuan anaripotiwa kupanga kukata rufaa katika mahakama ya juu, lakini taarifa za kina za hukumu hiyo hazijulikani.

Watafiti wenzake na wengine wanasema hana hatia na wanatoa wito kuwa aachiliwe mara moja.