Bunge la Georgia laidhinisha sheria ya ushawishi wa kigeni katikati ya maandamano

Bunge la Georgia limeidhinisha sheria iliyotungwa ya kudhibiti taasisi ambazo zinapokea fedha kutoka nje ya nchi hiyo.

Upigaji kura ulifanyika jana Jumanne wakati maandamano yakiendelea dhidi ya muswada wa sheria hiyo.

Sheria hiyo itazitaka taasisi zisizokuwa za kiserikali na vyombo vya habari vinavyopokea asilimia zaidi ya 20 ya fedha zao kutoka nje ya nchi hiyo kujiandikisha kama wakala wa ushawishi wa kigeni.

Vyama vya upinzani vinapinga vikali sheria hiyo, ambayo ililetwa na chama tawala. Vyama hivyo vinadai kuwa sheria hiyo ni sawa na sheria ya Urusi ambayo inatumika na serikali kudhibiti shughuli za taasisi na vyombo vya habari ambavyo serikali inaona si rafiki.

Jana Jumanne, wabunge walionekana kugombana ndani ya bunge.

Katika mji mkuu wa Georgia Tbilisi, kwa takribani mwezi mmoja wananchi wameandamana dhidi ya muswada wa sheria hiyo.

Rais wa Georgia Salome Zourabichvili alielezea nia yake ya kupinga kusaini sheria hiyo.

Lakini hata kama rais atairudisha sheria hiyo bungeni, chama tawala kina kura za kutosha za kupinga upinzani wake.