Maswali na Majibu: Jiepushe na kazi za muda za udanganyifu (2)

(2) Mikataba ya simu za smartphone iliyo kinyume cha sheria

NHK inajibu maswali yanayohusiana na kuhakikisha usalama katika maisha ya kila siku. Kumekuwepo na mfululizo wa visa ambapo wakazi wa kigeni nchini Japani wanahusika katika uhalifu baada ya kutuma maombi ya “kazi rahisi, zenye malipo ya juu” zilizowekwa kwenye mitandao ya kijamii. Katika mfululizo huu, tutakupatia mifano ya zile zinazoitwa kama kazi za muda za udanganyifu ambazo haupaswi kuzikubali. Katika kipengee hiki cha leo, tunaangazia mikataba ya simu za smartphone iliyo kinyume cha sheria.

Mwezi Januari mwaka 2024, mwanamke mmoja Mfilipino mwenye umri wa miaka ya arobaini alitiwa nguvuni kwa kushukiwa kuhusika katika udanganyifu baada ya kutia saini mikataba ya kununua simu za smartphone kwenye duka la kuuza vifaa vya kielektroniki na duka la simu za mkononi jijini Tokyo, kwa lengo la hasa kumpatia mtu mwingine.

Polisi wanasema mwanamke huyo alinunua simu hizo baada ya kuona tangazo la biashara katika mitandao ya kijamii linalosema atalipwa fidia ya takribani yeni 100,000 kwa kila simu ya smartphone atakayonunua. Baada ya kununua simu hizo, alizikabidhi kwa mwanachama wa kundi la uhalifu lililomwongoza kufanya manunuzi hayo. Baadaye, polisi walibaini kuwa kadi za SIM ndani ya simu hizo zilitumiwa ulaghai wa malipo ya kielektroniki.

Polisi wanasema kuna jumbe nyingi katika mitandao ya kijamii zinazojaribu kuwashawishi raia wa kigeni kuingia katika mikataba ya simu za smartphone na kumpatia mtu mwingine ama simu ya smartphone au kadi ya SIM kwa mabadilishano ya kulipwa fidia. Pia wanasema kuna visa vingi ambapo mwanachama wa kundi la uhalifu huambatana na mnunuzi na kupokea simu hiyo mara tu baada ya mkataba kutengenezwa.

Polisi wanasema ni kosa kuingia katika mkataba wa simu ya smartphone ulio kinyume cha sheria. Isitoshe, mnunuzi atawajibika kwa kuendelea kulipia simu hiyo na ada ya matumizi hata baada ya simu hizo kuuzwa tena kwa mtu mwingine. Polisi wanaonya watu kamwe kutokubali mwaliko wa kazi unaoonekana kuwa rahisi na wenye malipo ya juu.

Taarifa hii ni sahihi hadi kufikia Mei 14, 2024.