Israel yawaenzi waliofariki vitani Siku ya Kumbukumbu

Raia wa Israel jana Jumatatu walisimama ili kuwaenzi wenzao waliouawa katika vita au mashambulizi ya kigaidi. Katika Siku hii ya Kumbukumbu, wengi waliangazia mgogoro katika eneo la Gaza. Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu aliwaambia kuwa ushindi “utawahakikishia mustakabali wao.”

Watu kote nchini humo walisimama kwa dakika mbili kutoa heshima kwa vizazi vya waliofariki vitani. Netanyahu alizungumza wakati wa hafla iliyofanyika mjini Jerusalem, akiulezea mgogoro huo kuwa moja ya kuishi kwao. Alisema, “Ama sisi – Israel – au wao – madubwana ya Hamas, ama kuendelea kuishi, uhuru, usalama na ustawi, au uharibifu, mauaji, ubakaji na utumwa.”

Netanyahu alisema vita vya uhuru vya Israel “bado havijamalizika.” Aliongeza kuwa “Tutafikia malengo ya ushindi na kwenye kiini cha malengo hayo ni kurejeshwa kwa mateka wetu wote nyumbani.”

Netanyahu ameshutumiwa wakati wote wa mgogoro huo. Alishutumiwa tena wakati mtu alipovuruga hafla hiyo kwa kumzomea. Raia wengi wa Israel wana hasira kuhusiana na kushindwa kwa ulinzi kabla ya shambulizi la Hamas na kuhusiana na mapigano yaliyofuata.

Runinga ya Al Jazeera inaripoti kuwa wanajeshi wamewaagiza wafanyakazi katika hospitali moja iliyopo katika mji wa kusini wa Rafah kuhama. Wanajeshi hao wamezilazimu familia zilizopoteza makazi zilizokuwa zimetafuta hifadhi katika shule sita kuondoka.