Bangladesh inachunguza njia za kukabiliana na hatari zinazohusiana na joto

Bangladesh inatafuta njia mpya za kukabiliana na hatari zinazohusiana na joto baada ya kustahimili wimbi kubwa la joto mnamo mwezi Aprili.

Mwezi uliopita, serikali ya nchi hiyo ililazimika kufunga shule zote nchini kwa wiki nzima, wakati halijoto ilipopanda hadi nyuzi joto 40 za selsiasi na zaidi. Hatua hiyo iliathiri watoto wapatao milioni 30.

Msichana mwenye umri wa miaka 12 huko Dhaka aliiambia NHK kuwa ilikuwa vigumu kuhudhuria shule katika mazingira hatari kama hayo.

Kwa msaada kutoka Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto UNICEF, mamlaka ya afya ya Bangladesh imezindua Mwongozo wa Kitaifa wa Magonjwa Yanayohusiana na Joto. Mpango huo unalenga kuwalinda watoto na wale wanoweza kuathirika kirahisi, wakiwemo wanawake wajawazito dhidi ya hatari za kiafya zinazohusiana na joto. UNICEF inasema hatari ya kujifungua kabla ya muda ni asilimia 5 zaidi kwa kila ongezeko la nyuzijoto 1 ya Selsiasi.

Shirika hilo linasema kushughulikia magonjwa yanayohusiana na joto na kuweka vipaumbele kwa umahiri wa wataalamu wa afya ni muhimu ili kuleta mustakabali mzuri na wenye afya kwa watoto nchini humo.

Kulingana na makadirio ya hivi karibuni ya UNICEF, ifikapo mwaka 2050, watoto milioni 35.5 nchini Bangladesh wanatazamiwa kukabiliwa na wimbi kubwa la joto mara kwa mara. Hiyo ni asilimia 99 ya jumla ya idadi ya watoto kwa wakati huo.