Marekani kuongeza ushuru wa magari ya umeme ya China hadi 100%

Utawala wa Rais wa Marekani Joe Biden unasema utapandisha ushuru wa magari ya umeme ya China kutoka asilimia 25 hadi 100.
Ongezeko hilo la mara nne ni sehemu ya hatua zilizoongezwa dhidi ya bidhaa zinazonunuliwa kutoka China katika sekta mbalimbali.

Biden alisema katika taarifa yake jana Jumanne kwamba uzalishaji wa kupita kiasi wa bidhaa zilizopewa ruzuku na Serikali ya China unatishia makampuni na wafanyakazi wa Marekani.

Rais huyo alisema hatua hizo mpya zitalenga nyanja za kimkakati ambapo Marekani inafanya uwekezaji wa kihistoria. Ushuru pia utapandishwa kwa kiasi kikubwa kwa bidhaa zingine mbalimbali, ikiwa ni pamoja na betri za lithiamu na za umeme jua na semikondakta.

Kwa jumla, bidhaa zinazonunuliwa kutoka China zenye thamani ya dola bilioni 18 zinatarajiwa kuathirika.

Waangalizi wa mambo wanasema Biden anataka kuonesha kujidhatiti kwake kwenye viwanda vya ndani na ajira kabla ya uchaguzi wa rais mwezi Novemba. Wanasema China huenda ikajibu vikali.