Rais wa Urusi kutembelea China kwa ajili ya mkutano wa viongozi wakuu wiki hii

Rais Vladimir Putin wa Urusi atatembelea China wiki hii kwa ajili ya mkutano na Rais wa China Xi Jinping. Itakuwa ni ziara yake ya kwanza nje ya nchi tangu aapishwe katika muhula wake wa tano madarakani.

Wizara ya Mambo ya Nje ya China na ofisi ya rais wa Urusi jana Jumanne zilitangaza kuwa Putin atafanya ziara rasmi nchini China kesho Alhamisi na Ijumaa.

Putin atarajiwa kukutana na Xi jijini Beijing.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China alisema viongozi hao watajadili ushirikiano katika nyanja mbalimbali, wakati nchi hizo mbili zikiadhimisha miaka 75 ya uhusiano wa kidiplomasia..

Kwa kuichagua China katika ziara yake ya kwanza ya nje ya nchi kwenye muhula wake mpya madarakani, Putin anaonekana kulenga kuimarisha uhusiano katika kipindi hiki mgogoro ukizidi na Mataifa ya Maghaibi juu ya uvamizi wa Urusi nchini Ukraine.

China pia ni dhahiri inatafuta kuonesha uhusiano wake imara na Urusi ili kupinga shinikizo kutoka kwa Marekani.