Gari la UN lashambuliwa katika mji wa Rafah eneo la Gaza, mfanyakazi mmoja afariki

Umoja wa Mataifa, UN unasema mmoja wa wafanyakazi wake aliuawa na mwingine kujeruhiwa wakati gari la shirika hilo liliposhambuliwa katika mji wa Rafah uliopo kusini mwa Ukanda wa Gaza jana Jumatatu.

Msemaji wa UN aliwaambia wanahabari kuwa gari hilo lilikuwa likielekea katika hospitali moja iliyopo mjini Rafah liliposhambuliwa.

Aliongeza kuwa mfanyakazi aliyeuawa hakuwa Mpalestina ila ni mfanyakazi wake wa kimataifa. Utaifa wa mfanyakazi huyo haukuwekwa wazi.

Msemaji huyo alisema hicho ni kifo cha kwanza cha aina hiyo kuikumba UN tangu kuanza kwa mgogoro katika Ukanda wa Gaza mwezi Oktoba mwaka jana.

Katibu Mkuu wa UN Antonio Guterres ametoa wito wa kufanywa kwa uchunguzi kamili.

Vyombo vya habari vya Israel vinasema uchunguzi wa awali uliofanywa na jeshi la Israel umebaini kuwa mtu mmoja aliuawa na mwingine kujeruhiwa vibaya kutokana na kufyatuliwa risasi kwa gari la UN karibu na Mpaka wa Rafah.

Vyombo hivyo vinasema jeshi hilo bado linachunguza hali ambazo tukio hilo lilitokea, na kwamba “Si bayana ikiwa ufyatuaji risasi huo ulifanywa na wanajeshi.”

Hamas imeishutumu Israel kutokana na tukio hilo ikisema Israel ilishawashambulia wafanyakazi wawili wa kigeni – mwanamume na mwanamke – “ambao walikuwa wanasafiri katika gari la UN likiwa na bendera na alama za utambulisho wa UN.” Kundi hilo limesisitiza kuwa “Israel na Marekani ndizo zinazowajibika kikamilifu.”