Watu 3 washtakiwa nchini Uingereza kwa kusaidia idara ya ujasusi ya Hong Kong

Polisi mjini London wanasema watu watatu wameshtakiwa kwa kusaidia idara ya ujasusi ya Hong Kong.

Polisi wa mji huo walisema jana Jumatatu kwamba watu hao watatu wenye umri wa kuanzia miaka ya 30 hadi 60, walishtakiwa kwa makosa chini ya Sheria ya Usalama wa Taifa ya Uingereza.

Wanatuhumiwa kwa kufanya shughuli nchini Uingereza zilizolenga kusaidia idara ya ujasusi ya Hong Kong nchini Uingereza na kufanya uingiliaji wa kigeni.

Mmoja wa watu hao ni afisa katika Ofisi ya Uchumi na Biashara ya Hong Kong mjini London, kwa mujibu wa serikali ya eneo la Hong Kong.

Ubalozi wa China nchini Uingereza ulitoa taarifa inayosema China “inashutumu vikali utengenezaji wa Uingereza wa kinachoitwa kesi.”

Mwezi uliopita, mamlaka za Uingereza ziliwashtaki watu wawili kwa kutoa taarifa zenye madhara kwa China. Mapema mwezi huu, Uingereza ilitangaza kwamba itawafukuza wafanyakazi wa ulinzi wa Urusi kwa madai ya ujasusi.