Maswali na Majibu: Kujiepusha na kazi za vibarua za udanganyifu (1)

(1) Mauzo ya vitabu na kadi za benki

NHK inajibu maswali kuhusiana na usalama katika maisha ya kila siku. Kumekuwa na mfululizo wa kesi ambapo wakazi wa kigeni nchini Japani wanajihusisha na uhalifu baada ya kuomba “kazi rahisi na zinazolipa vizuri” ambazo hutangazwa kwenye mitandao ya kijamii. Washukiwa wote wa kazi zinazoitwa vibarua vya udanganyifu wanaweza kukamatwa au kurudishwa nchini kwao. Katika mfululizo huu, tutakushirikisha mifano ya kazi kama hizo ambazo hutakiwi kamwe kujihusisha nazo.

Moja ya kazi za udanganyifu zinazoajiri wageni ni mauzo ya vitabu na kadi za benki. Akaunti za benki mara nyingi hutumiwa baadaye kwa uhalifu kama utapeli na mauzo na manunuzi ya vitu hivyo ni kosa kisheria.

Polisi katika jiji la Tokyo wanasema kwamba wanaume wawili kutoka Vietnam walio katika umri wa miaka ya 30 ambao wanaishi mikoa ya Tokyo na Mie walimfanya mwanaume mwingine wa Vietnam anayeishi Osaka kuwatumia kadi yake ya fedha ya benki kwa mbadala wa fedha kupitia mtandao wa kijamii mnamo Mei 2022. Wote watatu walikamatwa kwa kukiuka Sheria ya Kuzuia Miamala ya Kihalifu.

Shirika moja Lisilo la Kujipatia Faida linalowasaidia raia wa Vietnam waishio Japani, Nichiestu Tomoiki Shienkai, linasema makundi ya kwenye mitandao ya kijamii ambayo wakazi wengi wa Vietnam wamejisajili yana machapisho yanayotoa wito wa mauzo ya akaunti za benki, yakitaja banki mahususi kwa jina. Shirika hilo pia linasema kuwa mara nyingi linasikia kuhusu raia wa Vietnam wakiuza vitabu na kadi za benki ili kupata fedha kabla ya kurudi nchini kwao.

Polisi wa Jiji la Tokyo wanaonya wakazi wa kigeni nchini Japani dhidi ya kazi haramu za vibarua, wakisema kuwa wanaweza kukamatwa au kurejeshwa nchii kwao ikiwa watajihusisha kazi kama hizo bila kufikiria vilivyo.

Taarifa hii ni sahihi hadi kufikia Mei 13, 2024.